Msimu wa 2009/10 wa ligi maarufu ya mpira wa kikapu ya nchini Marekani(NBA) umeanza rasmi hapo jana. Ni mwanzo wa mikikimikiki ya ushindani mkali ambao hutawala ligi hiyo.Kwa watanzania wengi, macho na masikio yao,watayaelekeza kwa Hasheem Thabeet ambaye kwa mapana na marefu atakuwa siyo tu anaitafutia timu yake ya Memphis Grizzlies ushindi,bali pia atakuwa akiipeperusha bendera ya nchi yake ya Tanzania kwa njia moja au nyingine.Habari za Hasheem zitakuwa sio tu za uchezaji bali pia jinsi ambavyo ni “ndoto iliyotimia” kwa kijana kutoka nchi ya “ulimwengu wa tatu” kama ya Tanzania kufikia kiwango cha kucheza katika ligi ya NBA ambayo hata huko Marekani kwenyewe,vijana wengi hutamani sana kufanya hivyo.Bila shaka jina la Tanzania litatajwa mara nyingi kuliko kawaida katika matangazo ya ligi hiyo.Ni kwa sababu ya Hasheem Thabeet,mtanzania wa kwanza kuchezea katika ligi hiyo.Haishangazi kuona kwamba watu wengi,wakiwemo viongozi wetu,wanajitahidi kuwa karibu zaidi na Hasheem Thabeet.Jina lake ni ishara ya ushindi.Ni lulu.Ingawa Hasheem hayupo bado katika “First Five” ya timu yake ya Grizzlies Memphis,bila shaka atacheza leo wakati timu yake itakapowakaribisha, Detroit Pistons (kutoka jijini Detroit,Michigan) mjini Memphis,Tennesse yalipo makao makuu ya Grizzlies Memphis.Watabiri wa mambo wanasema Hasheem tayari ameonyesha uwezo mkubwa wa kuzuia mirusho ya timu pinzani lakini wanashauri azidishe juhudi katika rebound.Bila shaka anasikia na atazingatia ushauri huo na pia wa makocha wake.Viwanjani inaungana na wote wanaomtakia kheri Hasheem.Tunaelewa kwamba mafanikio ya Hasheem ndio mwanzo wa mafanikio ya vijana wengine wengi wa kitanzania ambao naamini kabisa,endapo watapewa nafasi,wanaweza pia kufikia kiwango cha Hasheem.Kila la kheri HT.
No comments:
Post a Comment