Tuesday, May 25, 2010

KADI NYEKUNDU ILIYOLETA DHAHAMA ZAIRE

> Wakati bara la Afrika likiandaa michuano ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza, kuna jambo moja ambalo halijabadilika: wapenzi wa soka katika nchi za mashariki mwa Afrika na eneo la maziwa makuu wataendelea kuwaza na kuwazua waiunge mkono timu ipi, kwani hakuna nchi iliyofuzu kutoka eneo hilo.
Mara ya mwisho eneo hilo lilipowakilishwa katika kombe la dunia ilikuwa ni mwaka 1974 na nchi ya Zaire, ambayo leo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Zaire ilikuwa nchi ya pili kutoka bara la Afrika kushiriki michuano ya kombe la dunia baada ya Morocco, iliyoshiriki mwaka 1970, lakini Leopards, kama ilivyojulikana timu hiyo ya Zaire, ilikuwa timu ya kwanza kutoka kusini mwa jangwa la Sahara kufuzu kwa kombe la dunia.
Ingawa haijawezekana tena kwa nchi hiyo kufuzu kushiriki kombe la dunia, wachezaji waliokuwa katika timu hiyo ya mwaka wa 74 bado hujivunia hilo mpaka leo.
‘’Kombe la dunia ni kilele cha soka, ndicho kitu ninachojivunia maishani mwangu kwa kushiriki mwaka 74, tulikuwa nchi ya kwanza ya watu weusi kushiriki kombe la dunia, na ni fahari ya kukumbuka siku zote.’’ Mohamed Kalambay, aliyekuwa kipa wa akiba wa Leopards aliambia BBC.




Mohammed Kalambayi anajivunia kuwa mmoja wa wachezaji walioiwakilisha Zaire katika Kombe la Dunia 1974.
Leopards walifungwa mabao 14 katika mechi tatu bila wao kufunga hata moja. Katika mechi yao ya kwanza walifungwa 2-0 na Scotland, kisha wakabugizwa 9-0 na Yug
oslavia, na katika mechi yao ya mwisho wakafungwa 3-0 na Brazil.

Mwepu Ilunga alikuwa mlinzi katika timu hiyo, na ijapokuwa anaona fahari kwamba walifuzu kwenda kushiriki kombe la dunia, angali na machungu kuhusu waliokuwa maafisa wa shirikisho la soka Zaire, ambao anawalaumu kwa kuchukua pesa zilizotolewa na shirikisho la FIFA kwa wachezaji, kama mafao ya kushiriki.
‘’ Tulirejea nyumbani bila senti hata moja kama wachezaji. Kabla ya mchuano wetu dhidi ya Yugoslavia tulifahamu kwamba hatutalipwa, licha ya kufahamu kwamba FIFA walikuwa wameshawakabidhi fedha maafisa wetu. Kwanza tulikataa kucheza, na ilipolazimika kucheza, tulitembea tu uwanjani, na ndio sababu tukafungwa mabao 9.’’
Mwepu Ilunga anakumbukwa kutoka na kituko cha kuondosha mpira kuepusha free-kick.
Mwepu aanakumbukwa kote duniani kwa kituko alichofanya katika mechi yao iliyofuatia, dhidi ya Brazil. Brazil ilipata free kick hatua chache kutoka lango la Zaire, wachezaji wa Zaire wakaweka ukuta wa ulinzi. Lakini refarii alipopiga kipenga ili Brazil kupiga free kick hiyo, Mwepu aliondoka kutoka ule ukuta wa ulinzi, akaupiga ule mpira na kuuondosha nje.
‘’ Sijuti hata kidogo, nilifanya kwa kusudi. Nilitaka nipewe kadi nyekundu ili niondoke uwanjani. Kwa nini nicheze kwa faida ya maafisa wa chama cha soka cha nchi yetu waliochukua fedha za wachezaji zilizotolewa na FIFA?. Ila sikufaulu , refa hakunipa kadi nyekundu.’’
Bila kufahamika yaliyotokea, lawama nyingi zilielekezwa kwa kocha wa Leopards Blagoj Vidinic kutoka Yugoslavia. Lakini aliyekuwa naibu kocha msaidizi wa timu ya Leopards Kabamba Nicodem aliambia BBC kitendo cha maafisa wa chama cha soka kuwalaghai wachezaji ndicho kilisababisha matokeo mabaya.
Ujuzi na busara za watu kama Kabamba Nicodemu (shati jekundu) unaweza kusaidia kuirejesha Kongo katika mafanikio ya miaka ya 1970.
Kabamba anasema kwa sasa nchi hiyo ina wachezaji wazuri lakini kinachowafanya kushindwa kwenda kushiriki kombe la dunia ni ukosefu wa maandalizi bora.
‘’Ukosefu wa mipango mahsusi ndio umesababisha nchi ya Congo kushindwa kushiriki katika mashindano makubwa kama vile kombe la mataifa ya Afrika na kombe la dunia; bila maandalizi bora huwezi kufanikiwa katika jambo lolote’’. Anasema Kabamba.
Kuna hamasa kubwa ya mpira wa vilabu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo miongoni mwa mashabiki, klabu ya TP Mazembe kutoka mji wa Lubumbashi kusini mwa nchi ndio mabingwa wa sasa wa Afrika, na vilabu vingine kama AS Vita Club na DC Motema Pembe vinavutia wachezaji kutoka nchi zingine.
Timu ya taifa ya nchi hiyo ndiyo mabingwa wa taji la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani.
Haya yote yanaashiria uzito unaopewa soka katika Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, lakini swali linasalia kwa nini hawajaweza kurudi tena katika kombe la dunia tangu mwaka wa 1974?
Rais wa shirikisho la soka nchini Congo Constant Omar Selemani anasema ukosefu wa amani katika nchi, hali mbaya ya kiuchumi na kupuuzwa kwa soka ya vijana kwa kipindi kirefu kulikwamisha maendeleo ya soka katika nchi hiyo.
Constantine Omar Selemani rais wa shirikisho la soka la Congo ana jukumu kubwa la kuirejesha nchi hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia.
‘’Maendeleo ya soka yanakwenda kulingana na hali ya nchi, kijamii na kiuchumi. Wakati Zaire ilipofuzu kwa kombe la dunia mwaka wa 74 uchumi wa nchi ulikuwa mzuri, lakini tangu wakati huo kumekuwa na matatizo mengi katika nchi.’’
‘’Pia viongozi wa wakati ule walikosa maono ya kukuza wachezaji wapya. Wale wachezaji walioshiriki kombe la dunia walitaka kwenda kucheza soka ya kulipwa katika nchi za nje, lakini Rais Mobutu akawakataza, akawalazimisha kukaa nyumbani. Wengine waliacha kucheza, na kukawa hakuna mpango wa kukuza vijana wengine’’. Anaelezea Bw Selemani.
Rais huyo wa shirikisho la soka nchini Congo, ameahidi kwamba nchi yao itakuwepo kwenye mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.






Huyu ni celestine omar selemani moj kati ya wachezaji waliokuweepo wakati huo


No comments:

Post a Comment