Tuesday, May 18, 2010

Shangazi wa Obama rukhsa Marekani

Zeituni Obama
Shangazi wa Rais wa Marekani Barack Obama amepewa ruhusa kubaki nchini humo baada ya kuomba hifadhi ya kisiasa kwa mara ya pili.
Zeituni Onyango, aliyezaliwa baba mmoja na Bw Obama, anaendelea kuishi katika nyumba za umma huko Boston baada ya kukataliwa alipoomba hifadhi hiyo mwaka 2004.
Aliomba tena baada ya kujulikana hadharani kuwa anakaa kinyume cha sheria wakati wa kampeni ya Bw Obama mwaka 2008.
Wakati huo Bw Obama alisema hakujua kwamba shangazi yake alikuwa Marekani kinyume cha sheria.
Watu wanaotafuta hifadhi Marekani lazima waonyeshe kuwa wanateswa nchini mwao kwa misingi ya dini,asili, utaifa, kwa kutoa maoni ya kisiasa, au kujihusisha na kundi la utetezi.
Msingi wa kuomba hifadhi haukuwahi kuelezwa hadharani lakini wakili wake mmoja, Margaret Wong wa Cleveland, amesema Bi Onyango aliomba hifadhi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka jana kutokana na ghasia zilizotokea nchini Kenya.
Siku ya Jumatatu mawakili wake walisema alikuwa na mpango wa kuomba vibali vya kufanyia kazi na baadae kuomba mpango wa kutoa vibali kwa raia wa kigeni kuishi Marekani, 'green card'.
Rais wa Marekani alikutana na ndugu zake upande wa baba yake kwa mara ya kwanza alipotembelea bara la Afrika zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Akielezea safari yake hiyo, anamzungumzia Bi Onyango, ambaye humwita shangazi Zeituni, kama mwanamke mwenye kujali.
Bi Onyango aliitembelea familia huko Chicago kwa kutumia kibali cha utalii alichoalikwa na Bw Obama miaka 10 iliyopita na kutembelea marafiki wengine kabla ya kurudi Kenya.
Mwaka 2004 alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Bw Obama kama seneta lakini maafisa wamesema hakumsaidia kupata kibali cha utalii.

No comments:

Post a Comment