Tuesday, August 25, 2009

HONGERA COSOTA LAKINI BADO MNAKAZI YA KUWAPA ELIMU WASANII

MGAO WA SABA (7) WA MIRABAHA KWA WASANII WA FANI YA MUZIKI NA FILAMU
KAMPENI DHIDI YA UZALISHAJI NA USAMBAZAJI WA KANDA NA CD BANDIA (FEKI)
MGAO WA MIRABAHA
Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kinafurahi kuwatangazia wanachama wake na wasanii wa fani ya muziki na filamu kwa ujumla, kwamba mgao wa saba wa mirabaha umekamilika.
Wajibu wa kulipa mirabaha
Mirabaha ni pesa inayokusanywa kutoka kwa aina zote za biashara ambazo zinatumia kazi za muziki na filamu ili kuburudisha wateja kwa njia ya redio au luninga na kutoka kwa mashirika ya utangazaji.
Zoezi hili ni utekelezaji wa Kanuni za Utoaji Leseni kwa maonyesho ya Umma na Utangazaji za Mwaka 2003, Tangazo la Serikali Na. 328 la Tarehe 10/10/2003. Kanuni hizi zimetengenezwa chini ya kifungu cha 45 ikiwa ni utekelezaji wa Kifungu cha 48 cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki 1999, (Sheria Na. 7 ya mwaka 1999).
YUSTUS A.B MKINGA AFISA MTENDAJI COSOTA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI HABARI KUHUSU WIZI WA KAZI ZA WASANII
Kwa mujibu wa Kanuni hizi wamiliki wa biashara zifuatazo wanawajibika kulipa mirabaha. Biashara hizo ni pamoja na hoteli, baa, migahawa, maduka, kumbi za kukodisha, kumbi za disko, vituo vya utangazaji, wasambazaji wa matangazo kwa njia ya Kebo n.k.
Hali ya ukusanyaji wa mirabaha toka zoezi lianze
Kuanzia mwezi Mei 2006 hadi Disemba, 2008, COSOTA imekusanya jumla ya Sh. 306,327,040.33, ambapo migao sita imetolewa na kunufaisha jumla ya wanachama 956.

Mirabaha iliyokusanywa kuanzia Januari 2009
Katika kipindi cha Januari 2009 hadi Juni 30, 2009 kiasi cha Sh. 80,756,353.00/= kimekusanywa kama ifuatavyo:-
a) Makusanyo kupitia mawakala Sh. 24,256,353.00/=
b) Kamati ya vibali vya wasanii 600,000/=
c) Mabenki – 4,000,000/=
d) Redio Maria – 500,000/=
e) Juke Boxes (International Vending) 51,000,000/=
f) Juke Boxes (Kenice) 400,000/=
Jumla Sh. 80,756,000.00/=

Katika mgao huu wa saba zimegawanywa Sh. 80,256,353.00 jumla ya Sh. 500,000/= zilizokusanywa kutoka Redio Maria zinasubiri taarifa ya kazi zilizotumika na malipo kutoka vituo vingine vya utangazaji ili zigawanywe kwa pamoja.
Baada ya kutoa gharama ya ukusanyaji asilimia ya COSOTA na mfuko wa shughuli za kijamii za wanachama Sh. 50,548,163.66 zinagawanywa kwa wasanii kama ifuatavyo:-
a) Mgawanyo kwa wasanii wa fani ya muziki kutokana na maonyesho ya Umma Sh. 23,966,866.56.
b) Mgawanyo kwa wasanii wa fani ya maigizo kutokana na maonyesho ya umma Sh. 3,956,665.80.
c) Mgawanyo utokanao na Juke Boxes Sh. 22,624,631.30.
Jumla ya wasanii walionufaika na mgao huu kutokana na maonyesho ya umma ni 1088.
Jumla ya wasanii wa ndani na nje walionufaika na mgao utokanao na Juke Boxes 366.

1. Maendeleo ya ufuatiliaji wa mirabaha kutoka vituo vya utangazaji
Hadi sasa ni kituo kimoja tu ambacho kimelipa mirabaha. COSOTA imeshafanya majadiliano ya ana kwa ana na vituo vya utangazaji katika miji ya Dar es salaam, Iringa na Moshi. Wakati huo huo, vituo vyote nchini vimepelekewa fomu za madodoso ambazo zitaisaidia COSOTA kuweza kukokotoa viwango vya mirabaha inayopaswa kulipwa na vituo husika. Vituo vichache vimerejesha fomu hizo wakati vituo vingi bado havijarejesha. COSOTA inachukua nafasi hii kuwaarifu wamiliki wa vituo ambavyo havijarejesha fomu hizo kufanya hivyo ili wasanii waweze kunufaika kutokana na kazi zao kutumika na vituo hivyo.




1. Wito kwa watumishi wa serikali wanaokwamisha zoezi la ukusanyaji wa mirabaha katika maeneo yao
COSOTA inasikitishwa sana na kitendo cha baadhi ya watumishi na halmashauri na manispaa kukwamisha shughuli za ukusanyaji wa mirabaha na ulinzi wa Hakimiliki kwa ujumla katika maeneo yao. Wengine wamefikia hatua ya kuwaandikia barua wafanyabiashara wa maeneo yao, kwamba shughuli za COSOTA ni batili.

Wakati taratibu zinaendelea kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo, tunachukua nafasi hii, kuwaarifu watumishi wa aina hiyo, Wafanyabiashara na Umma na Watanzania, kwamba shughuli za ukusanyaji wa mirabaha ni halali na zinafanyika kwa mujibu wa Sheria za nchi.



. KAMPENI DHIDI YA UZALISHAJI NA USAMBAZAJI WA CD NA KANDA
BANDIA (FEKI)
1. Utangulizi
Mnamo tarehe 20/08/2009 COSOTA kwa kushirikiana na jeshi la polisi, wasanii na wadau wengine wa tasnia ya muziki na filamu, iliendesha operesheni ya kukagua maduka yanayouza kanda, CD na tumekamata kanda na CD bandia (Feki) mjini Dar es salaam. Oparehseni hiyo ilifanywa katika maeneo ya Kariakoo, Buguruni na Tabata.

2. Idadi ya kazi zilizokamatwa
a) Famous Video – Kipata / Nyamwezi
Katika duka hilo linalomilikiwa na mtuhumiwa Ayaj Amash Chavda ambapo mtuhumiwa amekuwa akitafsiri kazi za filamu Kihindi, idadi ya kazi zilizopatikana ni kama ifuatavyo:
(i) VHS (Video Cassettes) 4,076
(ii) DVD 932
(iii) VCD 185
(iv) VHS (Empty) 870
(v) VHS (mbovu) 33
Jumla – 6,096



Kutokana na maelezo ya mtuhumiwa, amekuwa akinunua Empty VHS kutoka Supershine – Zanzibar na VHS, DVD na VCD kutoka kwa Lufufu Kandala wa Vingunguti na Justine Limonga.

a) Adam Brothers / Abass Adam Salehe – Kariakoo CD 97
b) Kamugisha Shop CD – 14
c) Ana Maria DVD – 58
d) Moses Msigwa
(i) DVD – 12
(ii) VCD – 57
e) Kihiyo Athuman CD – 26
f) James Mbelwa CD – 6
g) Loveness Masonda – Tabata Kisukuru
Mtuhumiwa huyu alikamatwa kwa kosa la kuzalisha na kuuza DVD na VCD bandia za wasanii wa ndani na wan je. Kwa maelezo yake mwenyewe kazi hiyo anaifanya kwa kushirikiana na mumewe anayeitwa Johnson Michael na mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Msukuma.

Kazi na vifaa alivyokamatwa navyo ni kama ifuatavyo:
(i) Dukani kwake VCD na DVD 195 (kati ya hizo DVD 10 ni filamu za ngono).
(ii) Nyumbani kwake
- DVD, VCD na CD 31,500
- CD tupu (Empty) – 185
Pamoja na CD, mtuhumiwa huyu ambaye alikuwa anazalisha CD nyumbani kwake alikamatwa na vifaa vinavyotumika kutengenezea CD bandia na oda za kuuza Cd bandia kwa wateja wake zenye Jumla ya Cd 3,000 zenye thamani ya Sh. 15,000,000/=.

Hivyo basi Jumla ya CD na Kanda zilizopatikana katika operesheni hiyo ni kama ifuatavyo:
a) CD zilizorekodiwa – 33,219
b) CD Tupu (Empties) – 185
Jumla Cd – 33,404 zenye thamani ya Sh. 167,020,000/=
c) VHS – 4,076
d) VHS Tupu – 903
Jumla ya VHS = 4,979 zenye jumla ya thamani ya Sh. 9,958,000/= Jumla ya CD na VHS = 38,299





Vifaa vya kutengeneza CD bandia vilivyopatikana kwa mtuhumiwa Loveness Masonda ni kama ifuatavyo:-
a) Printa za rangi – 14
b) Kompyuta – 2 zenye jumla ya virekodio (CD Rom Drive) 16, nane kwa kila kompyuta.
c) Wino chupa 11
d) Vidao vya wino (cartridge) 55
e) Karatasi maalumu za kutolea nakala za picha (Inlays) – 700
f) Rim 1 ya karatasi
g) Vifungashio vya CD Paketi – 1
h) Mabomba ya sindano za kujazia wino – 4
Jumla ya thamani ya vifaa hivi inakadiriwa kuwa Sh. 14,222,000/=
Hivyo basi jumla ya thamani ya vitu vyote vilivyokamatwa siku hiyo vinakadiriwa kuwa ni Sh. 191,200,000/=




1. Operesheni ya kazi bandia katika kipindi cha kuanzia Januari 2009 hadi Agosti 19, 2009.
Katika kilichotajwa
(a) COSOTA imefanya zoezi kama hilo kwa msaada wa Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na wadau katika maeneo yafuatayo:-
(i) Dar es salaam
Ubungo, Mbezi beach, Mbagala na Bugurumi ambapo zilipatikana CD bandia 1,302.
(ii) Songea – CD 55 ziliharibiwa mbele ya vyombo vya habari baada ya mtuhumiwa kukimbia.
(iii) Kilimanjaro tarehe 27 – 29
Zilipatikana kazi bandia zifuatazo:-
- CD 575
- Kanda 41
- Vitabu 297 vya somo la Kimia (Secondary School Chemistry Book 1)
Vyote vipo mikononi mwa jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro.


(i) Arusha – 29 Aprili – 5 Mei, 2009.
- CD Bandia 1,450
- Kanda 104
Jumla 1,534

(a)Makampuni binafsi
Makampuni binafsi ya uzalishaji na usambazaji yalifanikiwa kukamata kazi zao bandia kama ifuatavyo:-
(i) STEPS
- Morogoro – CD 420
- Buguruni DSM – CD 800
- Ilala CD 400
Jumla – 1,620

(ii) Game 1st Quality Ltd
- Yombo Dovya – CD 400
- Buguruni – CD 20
- Tazara – CD 800
Jumla 1,220

(iii) MBC Hotmedia CD – 99

(iv) Msama Promotions
Dodoma, Mwanza, Morogoro, Shinyanga, Tabora na Singida Cd 1,300.

Jumla ya kazi bandia zilizokamatwa na COSOTA na wadau wengine katika kipindi hicho ni kama ifuatavyo:-

(a) CD – 9,401 zinazokadiliwa kuwa na thamani ya Sh. 37,505,000/=, Kanda 186, Sh. 279,000/= na vitabu 297, Sh 2,079,000/= vyote vinakadiliwa kuwa na thamani ya Sh. 39,863,000/=
Kwa maana hiyo kazi bandia zilizokamatwa kuanzia Januari 2009 hadi tarehe 24/08/2009 zinakadiliwa kuwa na thamani ya jumla ya Sh 231,063,000/=

1. Ukiukaji wa Hakimiliki
Kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, 1999 (Sheria Na. 7 ya mwaka 1999) kinasomeka kwamba “Mtunzi atakuwa na haki ya kipekee ya kutekeleza au kuidhinisha mambo yafuatayo kuhusiana na kazi
(a) utoaji nakala;
(b) usambazaji;
(c) ukodishaji;
(d) uonyeshaji kazi kwa umma;
(e) tafsiri ya kazi;
(f) toleo la kazi;
(g) utangazaji wa kazi;
(h) mawasiliano ya kazi, na
(i) uingizaji wa nakala kutoka nchi za nje

Kitendo chochote kinyume na kifungu hicho ni ukiukaji wa hakimiliki ambapo chini ya kifungu cha 42(a), adhabu ya mtu atakayepatikana na hatia yaweza kuwa kulipa faini isiyozidi Sh. milioni tano au adhabu ya kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uzalishaji na Usambazaji wa Kazi za Filamu na Muziki za Mwaka 2006, Tangazo la Serikali Na. 18 la tarehe 10/02/2006, COSOTa imepewa uwezo wa kuharibu kazi hizo mbele ya Umma baada ya siku 60 ikiwa aliyekamatwa nazo atashindwa kuthibitisha uhalali wa yeye kuwa na nakala za kazi alizokamatwa nazo.

Waliokamatwa katika Operesheni hizi ni wale ambao wamekuwa wakitoa nakala (kuzalisha), kusambaza(kuuza) na kutafsiri kazi pasipo kibali cha watunzi. Haijalishi kama mtuhumiwa anakiuka hakimiliki za wasanii wa ndani au wa nje. Wizi ni wizi tu, haijalishi kama unamuibia mtanzania au raia wa nje!

Chini ya kifungu cha 3(6)(a) na makubaliano ya kulindiana kazi na vyombo vya nje vyenye majukumu kama ya COSOTA, COSOTA imepewa uwezo wa kukamata kazi bandia zote, ziwe za ndani au za nje.

Nachukua nafasi hii kuwatahadharisha wauzaji wa CD na Kanda zenye kazi za nje, kuhakikisha kwamba wanapewa risiti na hao wanaowauzia. Kwa ujumla CD nyingi kutoka China ni bandia wala wauzaji wasidanganyike na CD zinazokuwa na filamu zaidi ya moja kwa kuwa hakuna mzalishaji halali mwenye akili timamu anayeweza kuweka filamu zaidi ya mbili katika CD moja.

Wakaguzi wa COSOTA wataendelea kukagua maduka yote yanayouza CD zenye kazi za watunzi wa nje kama wafanyavyo kwa kazi za ndani.

2. Motisha kwa Wasiri
Raia wema na wote wanaotembeza kanda mitaani (maarufu kama wamachinga), wanaarifiwa kwamba zawadi isiyopungua Sh. 200,000/= itatolewa kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazoisaidia COSOTA kukamata vifaa vinavyotumika kutengenezea CD bandia. Taarifa hiyo hiyo itolewe kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA pekee. COSOTA inahifadhi siri za wasiri.

3. Wito kwa Wasanii na Wanachama wa COSOTA
COSOTA inasikitishwa na ushirikiano mdogo inaopata kutoka kwa wasanii. Ni wasanii wachache sana ambao wamekuwa wakiisaidia COSOTA kwa nyakati mbalimbali. Wasanii walio wengi hawaji wanapoitwa na baadhi yao hudai malipo makubwa ambayo COSOTA haina uwezo wa kutoa.
Ikumbukwe kwamba jukumu la kwanza la kulinda hakimiliki ni la mwenye mali, yaani msanii mwenyewe kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha Sheria ya hakimiliki. COSOTA ina nafasi ya pili. Badala ya kushirikiana na COSOTA, kuitika wito na kufanya kazi na COSOTA, wasanii wengi wamebakia kulaumu na kulalamika tu.
Wakati huo huo naomba kuwapongeza baadhi ya wamiliki wa Makampuni ya uzalishaji na usambazaji ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kupiga vita uharamia.
4. Wajibu wa Wazalishaji, wasambazaji na wachapishaji kujisajili COSOTA.
Chini ya kifungu cha 47(b), COSOTA imepewa uwezo wa kutunza rejista za watayarishaji wa vihifadhia sauti zilizorekodiwa na vielelezo vya kusikia na kuona (kanda na CD), wachapishaji na wasambazaji wa kazi za muziki, filamu na maandishi.
Lengo la kifungu hiki ni kuiwezesha COSOTA kudhibiti utengenezaji na usambazaji wa kazi bandia, lakini pia kutambua alama za siri za usalama ambazo wahusika wanatumia ili kutambulisha kazi zao halali.
Pamoja na kuwatangazia kufanya hivyo, wengi wao wamekuwa wagumu kutekeleza maagizo hayo. Hali hiyo inaweza kusababisha COSOTA kukamata kazi halali kwa kudhania ni bandia.
Usajili huo ni muhimu zaidi kwa sasa ambapo COSOTA ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha matumizi ya stika ya kitaifa, kama alama ya usalama ya kutofautisha kazi halali na zile ambazo ni bandia.

Kwa niaba ya COSOTA napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuteua maafisa wa kushughulikia masuala ya hakimiliki ndani ya jeshi la polisi katika kila mkoa Tanzania bara na kwa Makamanda wa Polisi wa kanda maalumu ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro na wengine wote kwa kushirikiana na COSOTA katika kampeni dhidi ya kazi bandia. Maafisa hao wamekuwa msaada mkubwa kwa COSOTA katika kampeni dhidi ya kazi bandia(Feki).
Pamoja nao, shukrani ziuendee uongozi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kutoa wanafunzi ambao wanaendelea kutusaidia kwenye Kampeni hii, wasanii na wadau wote waliofanikisha zoezi hili, bila kusahau watumishi wa COSOTA ambao wamekuwa wanafanya kazi kwa moyo mmoja pamoja na vitisho wanavyopata kutoka kwa maharamia.











No comments:

Post a Comment