Thursday, April 29, 2010

Fulham yatinga fainali, Liverpool yatota



Fulham imeweka historia kwa kufika fainali ya ligi ya Europa baada ya kuichapa Hamburg 2-1.
Vijana wa Roy Hodgson hata hivyo walianza kwa kusuasua, baada ya kufungwa bao katika kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa adhabu kupitia Mladen Petric.
Hamburg wakicheza kwa uchu, kwa kuwa mchezo wa fainali utachezwa kwenye uwanja wao wa Nordbank, walidhibiti dakika 30 za mwanzo. Lakini kama ambayo wamekuwa wakifanya msimu huu, Fulham walizinduka na kubadili kibao.
Wakicheza bila ya mshambuliaji wao Bobby Zamora waliweza kubadili mchezo na kuibuka na ushindi.
Simon Davies alipachika bao la kwanza katika dakika ya 69, huku Zoltan Gera akipachika bao la ushindi dakika saba baadaye, na kuipeleka Fulham katika fainali.


Wakati huohuo Liverpool ilishindwa kutamba nyumbani dhidi ya Atletico Madrid.
Licha ya kushinda 2-1, Liverpool imetoklewa kwa sheria ya magoli ya ugenini. Katika mchezo wa kwanza Liverpool ilifungwa 1-0.
Alberto Aquillani ndie aliandika bao la kwanza kwa Liverpool na kulazimisha mchezo huo kwenda dakika za ziada.
Matumaini ya Liverpool kucheza fainali ya kombe la Europa yalipatikana baada ya Yossi Benyaoun kutikisa nyavu.
Hata hivyo Diego Forlan alizima ndoto za Liverpool, baada ya kupachika bao na kuizamisha Liverpool kwa goli la ugenini.
Fainali sasa itakuwa kati ya Fulham na Atletico Madrid itakayochezwa Mei 12.

No comments:

Post a Comment