Wednesday, April 28, 2010
UM wakubaliana kuwadhibiti maharamia
Maharamia wameendelea kuteka meli, licha ya jitihada za kimataifa kuimarisha doria bahari ya Hindi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa uwingi wa kura azimio linalokusudiwa kurahisisha kuwafungulia mashtaka maharamia watakaokamatwa katika pwani ya Somalia.
Rasimu ya azimio iliyoandaliwa na Urusi inatoa wito kwa mfumo wa sheria wa kimataifa kuimarisha mbinu za kukabiliana vitendo vya kiharamia.
Waraka huo unazisihi nchi zote kuunda sheria zinazopiga marufuku vitendo vya uharamia wa kuteka meli.
Maharamia waliokamatwa na majeshi ya majini ya kimataifa yanayolinda doria katika pwani ya Somalia, wamekuwa wakikabidhiwa kwa serikali za Kenya na Ushelisheli waweze kushughulikiwa kisheria.
Hata hivyo, kuna wasi wasi kwamba mfumo wa sheria wa Kenya umeelemewa na matatizo hayo.
Baadhi ya maharamia waliokamatwa wameachiliwa kwasababu ya utata wa kisheria kujua ni jinsi gani ya kuwafungulia mashtaka na kuendesha kesi zao.
Mahakama ya kimataifa
Azimio hilo linapendekeza Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, azingatie njia nyingine za kuwashughulikia na kuwafunga maharamia hao.
Hatua hizo ni pamoja na kuunda mahakama za kanda au kimataifa, au uwezekano wa mataifa kuanzisha mahakama zitakazoshirikiana na vitengo vya kimataifa.
KWA HISANI YA bbcswahili services
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment